×
MHE. NYONGO AFUNGA RASMI MASHINDANO YA SHIMMUTA 2024 NA KUAGIZA BAJETI ZA FEDHA ZA MICHEZO ZITUMIKE KWENYE MICHEZO NA SI VINGINEVYO.
02 Dec, 2024
Na Mwandishi wetu- Tanga Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo (Mb) amefunga rasmi mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) na kuagizaTaasisi zote zijitahidi kutenga bajeti ya michezo na kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Mashindano hayo yalitamatishwa jana Novemba 25, 2024 katika uwanja wa Popatlal Sekondari Jijini Tanga ambapo Mgeni Rasmi Mhe. Nyongo (Mb) alisema Ili kuhakikisha mashindano haya yanazidi kuwa bora na kuleta mvuto zaidi naelekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya michezo zitumike kwenye michezo. “Kuna baadhi ya Taasisi zinatenga bajeti na muda ukifika timu zao hazishiriki michezo ya SHIMMMUTA kwasababu fedha zinakuwa zimetumia kwenye mambo mengine, Rai yangu kwa wakuu wa Taasisi wote fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya michezo naomba zitumike kwenye michezo na si vinginevyo kwa sababu haya ni maagizo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan†amesema Dkt. Nyongo. Aidha Dkt. Nyongo amewapongeza washindi wa mashindano hayo na kuwahimiza wale ambao hawajashinda kuchukua fursa hii kujifunza na kujiandaa vyema kwaajili ya mashindano yajayo. Mwenyekiti wa SHIMMUTA Bi. Roselyne Mathew Massam amesema michezo hii ya SHIMMUTA 2024 ilianza tarehe 10 hadi 24 Novemba, 2024 ambapo jumla ya washiriki 4720 kutoka Taasisi 95 za Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi walishiriki, ukiliganisha na mwaka jana 2023 timu zilizoshiriki zilikuwa 57 tu. Ameongeza kwa kusema Mashindano ya SHIMMUTA 2024 yalihusisha michezo 12 ambayo ni Bao, Draft, Karata, Kamba, Kukimbia kwa Gunia, Darts, Pooltable, Riadha, Basketball, Football, Netball, Volleyball, ambapo Kauli Mbiu yetu ilikuwa ni "Michezo na Uwajibikaji: Tukiwahimiza Wanamichezo na Wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024. Naye, Katibu Mkuu wa SHIMMUTA Dkt. Maswet Masinda amewashukuru wakuu wa Taasisi mbalimbali ambao kwa nyakati tofauti wameendelea kutoa fursa na kuwaruhusu wanamichezo wa Taasisi zao ambao ni watumishi wa umma kushiriki mashindano ya SHIMMUTA.